MWANDISHI
wa habari ni mtu muhimu sana katika jamii, na wakati mwingine amekuwa
akitambulika kama Mhimili wa nne usio rasmi wa serilali, ukiacha Bunge,
Mahakama na Serikali.
Waandishi
wapo mstari wa mbele sana kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za
maendeleo, kupaza sauti juu ya kero mbalimbali zilizopo katika jamii hizo na
hata watatuzi wa hizo kero ama serikali au makundi mengine katika jamii hizo
kuona na kutafuta ufumbuzi wake.
Mwandishi
wa habari ni mtu ambaye huitumia kalamu yake ama kujenga kitu au mtu na mtu
huyo ama kitu hicho kuonekana ni bora zaidi kuliko vyote lakini pia kalamu hiyo
hiyo Mwandishi anaweza kuitumia kuboa kabisa kile alichokijenga kwa sifa nyingi
na jamii kuona huyu ndio mtu.
Hebu
ona sasa hivi mwandishi wa habari hasa Yule anayeaminika katika chumba fulani
cha habari alivyo ‘lulu’ katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa
Rais, Wabunge na madiwani.
Kila
mtu mwenye nia ya kutaka kugombea kuwania moja ya nafasi za uongozi anahaha
kupata mwandishi ambaye kama si kuamuandika vizuri gazetini au kumtangaza
vizuri na hao wapiga kura wake watarajiwa wakamsoma ili wamchague.
Ndio!
Na waandishi wa wazuri wapo wengi sasa wadau hapa wanazidiana kete tu na mtu
kutoka huku kwenda huku. Wapo wanaofanya kazi hiyo ya kuwapamba na kuwafagilia
watu ilimradi tu aione kesho yake bila kujadi maadili au laa lakini wapo wanaoifanya kazi hiyo kwa
kuzingatia maadili.
Mwandishi
wa habari amekuwa mbele sana katika kufanya mambo ya watu, lakini akijisahau
yeye mwenye matatizo lukuki yanayo mkabili. Hebu angalia wafanyakazi wa kampuni
fulani wagome kuhusiana na maslahi duni wanayopata au manyanyaso kwa mwajiri
wao uone kesho watakavyo andika magazetini na kutangaza, lakini wamesahau kuwa
wao ndio watu wa mwisho katika maslahi na hata hayo madogo wanayotakiwa
kuyapata hawayapati kwa wakati.
Hivi
sisi waandishi tumelogwa! Na kama ndio basi aliyetuloga hiyo tunguli kaitupa
baharini na na mganga mwenye kujua tiba yake kafa. Haiwezekani tumeshindwa
kujikingia kifua, ni waoga au nini kinatusibu hata kushindwa kupigania maslahi
yetu? Jamani haya maslahi tunashindwa hata kusaidiana nako tunashindwa?
Juzi
Kundi fulani la waandishi lisilo rasmi liliamua kuendesha kampeni ya kutafuta
fedha za kuwasaidia wenzao wanaumwa maradhi mbalimbali ikiwepo saratani.
Nilifika
katika tamasha hilo lililopewa jina la ‘Media Car Wash for Cancer’ pale viwanja
vya Leaders Dar es Salaam nikiwa
mshereheshi (MC) na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadic alikuwa
mgeni rasmi, pia tulikuwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Viongozi
hao walifika kutunga mkono katika harambee hiyo, mapema akimkaribisha mgeni
rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alisikitishwa sana na hali za
waandishi wa habari jinsi wanavyofanya kazi katika mazingira magumu, wakiwa na
maslahi duni pasipo na mikataba ya ajira. Ndio! Wengi wetu tunaishi kama
vibarua na hata hao walio ajiriwa au kuwa na mikataba ni duni.
Makonda
aliomba ridhaa ya Mkuu wa Mkoa kama vipi alibebe suala la kufuatilia maslahji
ya wanahabari kama alivyofanikiwa kwa madereva wan chi hii, ambao leo wamepota
mikataba inayoeleweka na mbioni kupatiwa bima za afya wao na familia zao.
Naamini
kabisa Makonda sakata la madereva alilijua kupitia waandishi na vyombo vya
habari.
Katika
harambee hiyo waandishi hawakujitokeza kwa wingi wao kama tunavyojuana idadi
yetu. Tumeshindwa kujitokeza kucheza ngoma yetu wenyewe je tumtarajie nani
atoke acheze? Sidhani kama Makonda atatosha bila sisi wenyewe kuonesha nia ya
kujisaidia.
Licha
ya umasikini wetu lakini wengi wetu tuna magari ambayo yangeoshwa pale na
kupata fedha, mbona pikipiki yangu Mkuu wa Mkoa na Mkuu wake wa Wilaya
waliiosha na kuingiza sh 150,000/=. Wachache waliokuja nawapongeza na waendelee
na moyo huo huo, tukijua fika leo kwao kesho kwetu.
Wanahabari
wakati umefika sasa wa kila mmoja wetu kujitoa katika mambo yetu na kuacha
kutumiwa na watu kwa faida zao. Tumekuwa watumwa wa wanasiasa hivi sasa lakini
ngoja washinde kama hata simu au sms yako atajibu.
Porojo hii imechapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Habarileo Julai 05,2015 kama Wazo la Mwandishi.
No comments:
Post a Comment