MD Digital

Sunday, March 17, 2024

MAKALA: WANANCHI KATA 22 WASIKILIZENI WAGOMBEA, MPIGE KURA

Wagombea wa vyama mbalimbali wakiangalia fomu za uteuzi wa wagombea walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugombea nafasi ya udiwani Kata ya Kimbiji iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Dar es Salaam. 
********"""
Na Mroki Mroki

TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Machi 20,2024 kuwa ni siku ya kupiga kura katika Uchaguzi Mdogo wa udiwani katika Kata 23 za Tanzania Bara.

 

Tume ilitangaza uchaguzi huo baada ya kuketi katika kikao chake cha Februari 15 mwaka huu na siku hiyohiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K  akatoa taarifa kwa umma juu ya uwepo wa uchaguzi huo mdogo.

 

Tayari mchakato wa Uchaguzi huo umeshaanza ambapo Februari 27 hadi Machi 4, 2024 wagombea walichukua fomu za uteuzi, uteuzi ulifanyika Machi 4,2024 na kampeni za uchaguzi zilianza Machi 5,2024 na zinaendelea hadi tarehe 19 Machi, 2024.

 

Hata hivyo, baada ya hatua ya uteuzi, Kata ya Nkokwa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ilipata mgombea mmoja tu aliyeteuliwa bila kupingwa hivyo hakutakuwa na kampeni kwenye Kata hiyo. Hivyo, uchaguzi utafanyika kwenye kata 22 zilizobakia.

 

Kata zitakazofanya uchaguzi huo mdogo ni Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Fukayosi(Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).

 

Nyingine ni  Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya  Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Mshikamano (Halmashauri ya Manispaa ya Musoma), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu) Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).

 

Katika Uchaguzi huu wa Kata 22, Vyama vya siasa 18 vimesimamisha wagombea 127 kati ya hao wanaume ni 89 na wanawake ni 38. Wagombea kutoka kwenye vyama hivyo walichukua fomu za uteuzi na kuzirejesha na hatimaye wakateuliwa kuwania nafasi hiyo.

 

Wagombea wa vyama mbalimbali wakiangalia fomu za uteuzi wa wagombea walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugombea nafasi ya udiwani Kata ya Kimbiji iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Dar es Salaam. 

Wagombea wote wameaminiwa na kupewa ridhaa na vyama vyao vya siasa kuwania nafasi zilizowazi,  kwa kufanya hivyo, vyama hivyo vya siasa  vimewatendea haki wanachama wao na wananchi kwa ujumla kwa kuwa wamepata haki ya kikatiba ya kugombea lakini pia wanachama na wananchi, watapata haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.

 

Wagombea walioteuliwa na Tume ni wale waliopendekezwa na vyama vyao vya siasa kugombea kiti cha udiwani ambapo pia walijaza na kuwasilisha fomu za uteuzi katika Ofisi za Uchguzi katika Kata husika.

 

Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata walisimamia vyema majukumu yao ya kutoa fomu za uteuzi. Fomu za uteuzi za wagombea wote ziliwasilishwa siku ya uteuzi kabla ya saa kumi kamili (10:00) jioni.

 

Wagombea hawa wote siku ya uteuzi walijaza na kusaini mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Fomu Na. 10 ya maadili ya uchaguzi.

 

Wagombea hawa walijaza fomu hizo   kukiri kuheshimu na kuyazingatia maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa na  viongozi wa vyama vyao mwaka 2020 wakati wa uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara.

 

Uwepo wa maadili ya Uchaguzi unalenga hasa kuwa na uchaguzi huru, wa haki, uwazi na wa kuaminika. Na kwamba amani, ustawi wa nchi, usalama wa raia, uhuru wa vyama vya siasa na utii wa sheria , kanuni na taratibu za uchaguzi ndio msingi wa uchaguzi ulio huru, haki na wenye kuzingatia ushiriki wa makundi yote ya jamii katika uchaguzi.

 

Vyama vya Siasa, Serikali na Tume walikubaliana kuwajibika kuyatekeleza Maadili hayo yanayotokana na kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343. Viongozi hao kwa pamoja walisema “Tutafanya jitihada za wazi kuhakikisha Maadili haya yanajulikana na kuheshimiwa na wagombea pamoja na wanachama wote wa vyama vya siasa”.

 

Sheria, Kanuni na miongozo yote iliyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 bado inatumika na kufuatwa na vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchagzi na Serikali katika chaguzi hizi ndogo za udiwani.

 

Tayari Kampeni za uchaguzi zimeanza tangu siku moja baada ya uteuzi na zitaendelea hadi siku moja kabla ya siku ya kupiga kura.

 

Wakati wote wa kampeni wagombea wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni za uchaguzi, Maadili ya Uchaguzi na ratiba za kampeni.

 

Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi na ratiba za kampeni utasaidia katika kuweka uwanja sawa katika kipindi chote cha kampeni na siku ya uchguzi.

 

Vyama vya Siasa na wagombea pamoja na wafuasi wao wanapaswa kuepuka kufanya siasa za fujo na za vitisho dhidi ya upande mwingine.

 

Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, imepewa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia taasisi au asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo.

 

Tume itatoa elimu kwa wananchi katika maeneo yote ambayo yanafanya uchaguzi mdogo. Lakini pia zipo asasi ambazo zimepewa kibali na Tume kutoa elimu hiyo kwa baadhi ya maeneo.

 

Elimu hiyo inayotolewa ni ile ya kumuwezesha Mpiga Kura kutambua sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ikiwa ni pamoja na utaratibu mzima wa kufunguliwa na kufungwa kwa vituo vya kupigia kura. 

 

Lakini pia elimu hiyo itasaidia kutoa hamasa kwa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba katika kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.

 

Ni muhimu wananchi katika maeneo yote yanayofanya uchaguzi mdogo wakajitokeza kwa wingi kusikiliza sera za vyama na wagombea kisha kwa utashi wao wachague viongozi wanaowafaa kujaza nafasi zilizowazi katika Kata 23 za Tanzania Bara.

 

Mwandishi wa Makala haya ni Afisa Habari Msaidizi Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Thursday, January 25, 2024

MTOTO AKAA ICU SIKU 60, HOSPITALI IKITUMIA MILIONI 10,100,000 KUMTIBU

 
Na Raymond Mtani-BMH          
Novemba 11, 2023, Bi. Janeth (35), mkazi wa Manyoni Singida, alifika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) baada ya kukaa siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni akiimuuguza mwanaye aliyepatwa “degedege”.
 
Siku hiyo, ikawa safari ya siku 60 za mtoto wake huyo mwenye umri wa miaka 4 kwenye Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda ya Kati.
 
“watu walikuwa wanakuja, wanaruhusiwa wanamuacha mwanangu, wakati mwingine anabaki peke yake”.  alisema Bi. Janeth.
 
Dkt. Venance Misago ni Bingwa wa Ganzi na Wagonjwa Mahututi, na Mkuu wa Idara ya Huduma za Uangalizi Maalumu BMH amesema, Moyo wa mtoto huyo ulisimama ghafla (cardiac arrest) mara nne (4) ndani ya siku 60 mtoto huyo alipokuwa ICU.
 
“aligundulika kuwa na maambukizi kwenye Ubongo (meningitis), hali iliyokuwa inasababisha apoteze fahamu mara kwa mara” alieleza Dkt. Misago.
 
Aidha, Dkt. Misago amesema kuwa kwa kawaida mgonjwa hukaa katika Chumba cha uangalizi maalumu siku 3 hadi 14 lakini maambukizi aliyokuwa nayo mtoto huyo yalisambaa kiasi cha kusababisha presha kushuka na kupelekea Moyo kusimama (septic shock) mara kwa mara.
 
Ingawa hali hiyo haikuwa rahisi kwa Bi. Janeth, hakusita kumshukuru Mungu, Madaktari na Wauguzi waliyomhudumia mwanaye.
 
“...nilipitia wakati mgumu kiasi cha kukata tamaa, namshukuru Mungu kwa kumponya mwanangu, nawashukuru Madaktari na wauguzi kwa kumpambania mwanangu” alieleza Bi. Janeth kwa furaha.
 
Kwa mujibu wa Awadhi Mohamed, Mkurugenzi Msaidizi huduma za Usitawi wa Jamii Hospitali ya Benjamin Mkapa imetumia Shilingi 10, 100,000 kugharamia dawa, vifaa tiba na chakula kwa kipindi chote cha siku 60 Mtoto wa Bi. Janeth alipokuwa ICU.
 
Kupona kwa mtoto huyo ni kielelezo cha faida za uwekezaji katika sekta ya Afya nchini, hasa mapinduzi yanayofanywa katika kuboresha huduma za Wagonjwa Mahututi.
 
Ingawa, wakosoaji wa serikali hasa Wizara ya Afya wamekuwa na jicho la kutoridhishwa na hatua za maboresho hususani kasi ya utekelezaji na ubora wa huduma, historia ni mwalimu mzuri.
 
Historia inakili kwamba, maboresho ya huduma ni mchakato, huduma za Afya nchini haziwezi kutokea ghafla mithili ya kimbunga, zinapitia mkondo huo huo wa mchakato wa maboresho ikiwa ni pamoja na huduma za ICU.
 
Mathalani, taarifa za Maktaba ya Historia ya Tiba ya Nchini Marekani zinadokeza mchakato wa maboresho ya huduma za ICU katika nchi za Ulaya ulianza kwa kanuni za kutenga majeruhi wa vita vya Crimean kwa kuwaweka mahututi jirani na vituo vya wauguzi (nursing stations) ili wapewe uangalizi maalumu.
 
Hiyo ilikuwa 1854, maboresho hayo yaliyohamasishwa na Bi. Florance Nightingale kusaidia kuokoa Maisha ya Majeruhi wengi wa vita, Ulaya ilisubiri karibu miaka 100 na mlipuko wa Polio kuwa na ICU ya kwanza, iliyojengwa 1953 huko Copenhagen, Denmark.
  
Hali hii ni tofauti na Tanzania, kwa mujibu wa Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, alipowasilisha Makadiliyo ya bajeti, mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, aliliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu hatua kubwa zilizopigwa katika huduma za Wagonjwa Mahututi.
 
Waziri huyo wa Sekta ya Afya, alinukuliwa Mei 12, 2023 akisema kuwa baada ya shambulio la Uviko 19, serikali imeweza kuongeza wodi za Wagonjwa Mahututi kutoka 45 had 258 ndani ya kipindi cha miaka 2, yaani 2020 hadi 2023.
 
“Tunaweza kulaza wagonjwa mahututi 1000 kila siku nchini” alisema Mhe. Ummy Mwalimu.
 
Hapana shaka, kama ilivyo kwa Mtoto wa Bi. Janeth, maboresho ya huduma za ICU yaliyofanyika katika kipindi hicho cha miaka 2 yamesaidia kuokoa maelfu ya Maisha ya Watoto na watu wazima waliyokumbwa na changamoto mbalimbali za kiafya zilizowalazimu kuhitaji ICU.
 
Mwaka 2020, Hospitali ya Benjamin Mkapa ilikuwa na Wodi ya Wagonjwa Mahututi yenye vitanda 6 pekee, lakini kupitia maboresho hayo, hadi Makala haya yanaandi.kwa, Hospitali hiyo ina Wodi mbili za wagonjwa Mahututi zenye vitanda 22.
 
Kwa mujibu wa Dkt. Misago, vitanda hivyo vina mashine za kusafisha mfumo wa hewa (Suction Machine), mashine za kusaidia kupumua (Ventilator), mashine za kusaidia Moyo, Figo na Kuzuia damu Kuganda (Syringe pump and Infusion Pump) pamoja na mashine za uangalizi wa mwenendo wa matibabu ya Mgonjwa (Monitors).
 
Hali hiyo, inasaidi kuokoa Maisha ya wanchi wengi wenye kuhitaji huduma hizo kwa uhakika, kumbuka iliichukua Ulaya miaka 99 kupata ICU ya kwanza, huku Tanzania ikijenga ICU zaidi ya 200 ndani ya siku 730.