MD Digital

Tuesday, July 14, 2015

TUSILAUMIANE, POLISI JICHUNGUZENI NA UVAMIZI HUU



USIKU wa kumkia jana Jeshi la Polisi lilipata pigo kubwa kufuatia vifo vya askari wake 4 na mwingine kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha kuvamia kitio Kikuu cha Polisi Stakishari Ukonga.

Kituo hiki ni kikubwa kwani ni Kituo Kikuu cha Wilaya ya Kipolisi ya Ukonga, katika Kanda maalum ya Dar es Salaam ambacho kina wajibika katika mkoa wa Kipolisi Ilala.

Naandika hapa huku nikiwa na majonzi na huzuni kubwa kufuatia vifo vya wapendwa wetu hawa. Pia walikufa raia watatu huku mmoja akihisiwa kushiriki katika tukio hilo na kuuwawa na wenzake hao.

Hili la Ukonga Stakishari limetokea wakati bado hatujasahau yaliyotokea katika vituo vingi vya Polisi kama Newala, Ikwiriri, Kimanzichana na Bukombe ambapo iliripotiwa jumla ya silaha 41 zimeporwa na baade 32 kupatikana lakini pia askari zaidi ya 5 kuuwawa. 

Tukio hili la Ukonga Stakishari limetokea ikiwa imepita miezi minne tangu Rais jakaya Kikwete alipozungumzia wimbo hilo la mashambulizi kwenye vituo vya polisi nchini.

Rais Kikwete akihutubia taifa miezi minne iliyopita, alisema kuwa  polisi wanachunguza sababu ya uvamizi huo. Bila shaka na ninaamini kuwa uchunguzi huo ulisha baini sababu ya uvamizi huo.

Lakini jana tumeshuhudia tena jinamizi hilo la uvamizi na uwaji wa Polisi vituoni nchini ukianza tena baada ya kimya cha muda mrefu na wananchi tuliamini kudhibitiwa kwa hali hiyo.

Japo kuwa Wakuu wa Chombo hicho cha Ulinzi wa raia na mali zake wanatoa hofu kwa wananchi kuwa watulivu na amani lakini, nitakuaje na amani kama chombo cha kunitunzia hiyo amani kinashambuliwa na walinzi hao wa amani kuuwawa ilhali wanamafunzo na silaha za kutosha?.
 
Kituo cha Polisi si sehemu ya masihara hata kidogo hasa ukizingatia unyeti wa Jeshi la Polisi hapa nchini.

Ipo haja ya Polisi wakiwa vituoni humo wakae kwa hadhari kubwa, na pia kuwa tayari kwa lolote wakati wowote.

Jeshi la Polisi ni mhimili wa nchi katika suala zima la ulinzi wa raia na mali zao,  hivyo tunatarajia kuona juhudi za makusudi zikifanyika kuhakikisha vituo vyote vya jeshi hilo siyo tu vinalindwa, bali pia vinawekewa mazingira ya kuwawezesha askari polisi kufanya kazi zao bila hofu ya kuvamiwa. 

Ni kweli vipo vituo ambavyo havina mazingira rafiki ya kazi na si salama lakini kwa kituo kikubwa kama Stakishari Ukonga, inatubidi kuamka sasa.

Si wakati wa kulaumiana au kunyoosheana vidole, lakini kitendo cha kuvamiwa na majambazi na kuporwa silaha, huku baadhi ya askari wake wakiuawa na wengine wakiachwa na vilema vya maisha si jambo dogo, mi nadhani kuna sehemu pia ndani ya jeshi letu tunapaswa kuliangalia, ama ni askari kujisahau na kumwamini kila mtu au hujuma miongoni mwa askari.

Nasema hujuma kwa maana ya kwamba, nirahisi mtu kufika kituo cha polisi na kufanya atakayo lakini kufika hadi chumba maalum cha kuhifadhia silaha na kuzichukua kama zake kirahisi tu nasema iko namna.

Chumba hicho daima huamini kuwa ni chumba kilicho na ulinzi mkali na pia huwa na milango imara ambayo itamfanya mtu yeyote anaetaka kufanya uhalifu humo kukamatwa kabla ya kufikia adhma yake hiyo. 

Ijapo kuwa vituo vya polisi ni nyumba ya wahalifu lakini siamini kama wahalifu hawa tuwafikishapo vituoni humo huwatembeza kila kona ya majengo yetu kiasi siku wakija wanajua kabisa hamari ni wapi na funguo hukaa wapi au mlango ule ukiupiga teke unafunguka.

Huenda wanakuwa na wenyeji, katika hili IGP Mangu, na maofisa wako hamna budi kuchunguzana kimaadili na mienendo ya askari wetu siku hadi siku na kubaini wale walio katika mstari na walio nje.

Wakati umefika sasa wa jamii kutoa taarifa za uhalifu kwa Jeshi la Polisi kwa lolote ambalo unalihisi si salama. 
POROJO Hii imechapishwa leo katika Gazeti la HABARILEO 
kama WAZO LA MWANDISHI.

No comments: