Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi
na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akiendesha mjadala kwa
wanakijiji wa Ololosokwan na vijiji vingine vinavyozunguka kijiji
hicho,viongozi wa halmashauri, viongozi wa kimila, viongozi wa vijiji na
wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya, elimu na uchumi ikiwa ni
maandalizi ya kuupokea mradi wa kijiji cha kidigitali Ololosokwani
wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.
Afisa
mipango ya Elimu wa Shirika la UNESCO, Bi. Jennifer Kotta (kulia) akiwa
kwenye majadiliano na baadhi ya wanakijiji wa Ololosokwan kuhusiana na
changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu na nini kifanyike
kuboresha sekta ya elimu kwa ujumla katika kijiji hicho na kuishirikisha
halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro katika maandalizi ya kupokea mradi
wa kijiji cha kidigitali.
********
Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
SHIRIKA
la Elimu ,sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, limeanza
maandalizi ya kuumilikisha mradi wa kijiji cha digitali cha Ololosokwan
kwa wananchi wa kijiji hicho kwa kuendesha warsha ya siku mbili ya
kutambua vipaumbele vya wananchi vitakavyoingizwa katika mradi huo.
Vipaumbele hivyo ni katika elimu, afya na uchumi. Warsha
hiyo ilishikirikisha wanakijiji wa Ololosokwan na vijiji vingine
vinavyozunguka kijiji hicho,viongozi wa halmashauri, viongozi wa kimila,
viongozi wa vijiji na wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya, elimu na
uchumi.
Katika
majadiliano yao wananchi walitambua changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na mazingira
na mfumo wa utamaduni walionao wakazi wa eneo hilo.
Wakazi hao ambao
ni wafugaji wenye kuheshimu mila na utamaduni wa kimasai na mfumo wa
maisha wamesema kwamba lugha inayotumika katika kufundishia ni tatizo na
ingawa wana shule mbili za msingi na sekondari lugha ya Kiswahili ni
tatizo na wakifika sekondari lugha ya kiingereza nayo inakuwa tatizo.
Aidha
walisema kutokana na wazazi kutokuwa na elimu hawaoni sababu ya
kuwafanya watoto wao wenye maarifa makubwa kwenda shule na badala yake
hao wanaoelewa vitu hupelekwa kuchunga au wale wenye umri mdogo wa kike
huolewa.
Warsha hiyo pia ilibainisha tatizo la afya ya wanawake na watoto, ndoa za utotoni na magonjwa ya zinaa ya kuambukiza.
Kijiji hicho cha
digitali ambacho ni nadharia ya Samsung katika kurejesha faida kwa umma
kitakuwa na huduma mbalimbali ambazo zikiunganishwa na haja ya wananchi
zitasaidia kubadili maisha ya wamasai na kuondokana na utegemezi wa
mifugo pekee na kutambua thamani yao katika rasilimali zilizopo katika
maeneo yao.
Warsha
hiyo ambayo imesimiwa na wataalamu kutoka UNESCO imelenga kuwafungua
macho na kuwashirikisha wananchi kuhusu mradi huo mkubwa wa aina yake
nchini na duniani.
Kijiji cha dijitali nchini Tanzania ni cha nne cha kwanza kikiwa nchini Afrika Kusini, kingine Gabon na Ethiopia.
Kijiji hicho ili
kiwe endelevu wananchi wanaohusika wanatakiwa kuelewa mradi huo kuweka
vipaumbele vyao na kuangalia jinsi ya kutumia mradi huo katika kukabili
changamoto zinazowakabili kwa sasa.
Katika
majadiliano kwenye ngazi za elimu wananchi walielezea haja ya
kushawishi wamasai kuanza kujifunza Kiswahili na Kiingereza ili kuweza
kufuatilia kwa karibu masomo na pia kuwepo kwa sheria ndogo ili kuzuia
utoro wa wanafunzi kwa ajili ya kwenda kuchunga mifugo na pia kuolewa
mapema kwa mabinti.
Mathias
Herman, mratibu wa program za Afya , UNESCO, alisema kwamba pamoja na
kwamba kijiji hicho kitakuwa na zahanati na huduma za mawasiliano ya
tiba (telemedicine) hamasa kubwa inatakiwa kutolewa ili wananchi waweze
kutumia huduma hizo kwani kwa sasa wamejikita zaidi huduma za waganga
wa jadi.
Alisema katika
warsha kulielezwa kuwa kukosekana kwa madaktari katika zahanati zilizopo
kijijini hapo kumefanya watu wengi kuendelea kuamini waganga wa jadi na
kujifungulia huko hali ambayo imezaa kuwapo kwa idadi kubwa ya wanawake
wanaokufa wakati wa uzazi na pia watoto wasiopata chanjo.
“Wakifika
hakuna madaktari hawawezi kuamini huduma hii wakati kuna waganga wa
kienyeji na wakunga wa kienyeji” alisema Mathias na kuongeza kuwa katika
warsha ilihimizwa kwamba watu watambue tatizo lililopo la kiafya
linalosababishwa na mfumo wa mazingira na maisha ya wafugaji na
kuhakikisha kwamba huduma zinazoletwa zinatumiwa vyema.
Aidha
alisema kuwapo kwa kiwango kikubwa cha maambukizi ya magonjwa ya zinaa,
ndoa za utotoni na mimba katika umri mdogo ni sehemu ya matatizo ambayo
yanaaminika kwamba yanaweza kutanzuliwa kwa kutolewa elimu na
kushawishi wakubwa wa mila kutambua nafasi zao na elimu ya kisasa katika
kushughulikia changamoto za kiafya.
“mila
na heshima kwa wakubwa wa mila kumefanya wamasai kutegemea tiba za
asili na mfumo wa asili wa kuendesha maisha bila kujua athari kwao ziwe
hasi au chanya” alisema Mathias kauli iliyoungwa mkono na Mkurugenzi
Mkazi wa UNESCO, Zulmira Rodrigues ambaye alisema kunahitajika sana
ushirikiano wa jamii, viongozi, wazazi kuhakikisha kwamba kijiji
kinafanikiwa na kuwa cha kupigiwa mfano.
Kijiji
cha Ololosokwan kilichopo Loliondo, wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha
kikiwa na watu 9000 kupitia mradi huo kitapewa pia mbinu za kuimarisha
soko la utalii, kulitambua na kulitumia kwa manufaa yao na pia elimu ya
ubunifu ambayo itawafanya wanawake wanaotengeneza urembo mbalimbali
kuweza kumudu soko la utalii na la kawaida.
Aidha mradi huo
utafikisha umeme na elimu kwa njia ya Tehama huku, elimu hiyo ya Tehama
ikikusudiwa kutumika kutoa elimu ya darasani kwa wanafunzi ambao wapo
machungani.
Mfumo
wa wamasai ambao umejengwa katika utamaduni na kuthamini mifugo
unatakiwa kubadilishwa kwa wazazi kupewa elimu ya kuwawezesha kutambua
umuhimu wa elimu kwa watoto wao.
Afisa
Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la
Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Bw. Al Amin Yusuph akiendesha
mjadala na baadhi ya wanakijiji wa Ololosokwan kuhusiana mradi wa kijiji
cha kidigitali na kuuboresha ili kutatua matatizo ya wananchi pamoja na
kuwapata taarifa za maendeleo kupitia redio jamii ya Loliondo FM
inayofadhiliwa na UNESCO ikiwa ni katika maandalizi ya kuupokea mradi
huo wa kijiji hicho unaotarajiwa kuwasili hivi karibuni kijijini hapo.
Afisa
Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias
akiongoza mjadala wa nini kifanyike katika kuboresha sekta ya afya na
changamoto zinazowakabili wanakijiji wa Ololosokwan kwa ajili ya
maandalizi ya kuupokea mradi wa kijiji cha Kidigitali unaoendeshwa na
UNESCO kwa kushirikiana na kampuni ya Ki-elektroniki ya Samsung
unaotarajiwa kuwasili mapema mwezi februari kijijini hapo. Wa pili
kushoto ni Mratibu wa Taifa wa tiba asilia na mbadala katika Idara ya
Tiba Wizara ya Afya na ustawi wa jamii. Dkt Liggy Vumilia.
Afisa
mipango ya Elimu wa Shirika la UNESCO, Bi. Jennifer Kotta akiwasilisha
kazi ya kikundi chake baada ya kujadiliana na wanakijiji wa Ololosokwan
katika kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni maandali ya kupokea mradi wa
kijiji cha kidigitali kinachotarajiwa kuwasili hivi karibuni kijijini
hapo.
Mmoja
wa washiriki wa kikundi kilichokuwa kikijadili masuala ya utamaduni na
utalii akiandika changamato mbalimbali zinazowakabili wakinamama
wakimasai wanaofanya biashara za urembo wa kimasai kwa watalii
wanaotembelea hifadhi ya Ngorongoro.
Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi
na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akishiriki kwenye
mjadala na wanakijiji wa kijiji cha Ololosokwan katika maandalizi ya
kupokea mradi wa kijiji cha kidigitali unaotarajiwa kuwasili mapema
mwezi februari kijiji hapo.
Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi
na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akisaini mkataba wa
kukabidhiwa ardhi iliyotolewa na serikali ya kijiji kwa ajili ya mradi
wa kijiji cha kidigitali huku tukio hilo likishishudiwa na uongozi wa
juu wa serikali ya kijiji, wataalam kutoka UNESCO na halmashauri ya
wilaya ya Ngorongoro pamoja na wanakijiji.
No comments:
Post a Comment