Na Michael Komba
NDONDI ni miongoni mwa
michezo ambayo imewahi kuitangaza vilivyo Tanzania katika anga ya kimataifa,
kama ilivyokuwa kwa riadha.
Mabondia ambao waliwahi
kuipeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika mashindano mbalimbali ya
kimataifa, ni Michael Yombayomba, Habibu Kinyogori, Titus
Simba, Emmanuel Mlundwa, Rashid Matumla na wengineo.
Soka ambayo ndio mchezo
unaopendwa na kupewa kipaumbele zaidi hapa nchini, haujawahi kuiletea Tanzania
mafanikio yoyote, zaidi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika
mwaka 1980 nchini Nigeria.
Zaidi ya mafanikio
hayo, timu yetu ya Taifa, Taifa Stars na hata klabu zetu, zimebaki kuwa ‘kichwa
cha mwendawazimu’ katika michuano mbalimbali ya kimataifa.
Angalau riadha na
ndondi zimefurukuta kwa kutwaa medali katika mashindano makubwa kama michezo ya
Olimpiki na Michezo ya Afrika (All Africa Games’.
Pamoja na hilo, mchezo
wa ndondi bado unaonekana kupewa kisogo na wadau kwa kushindwa kuboresha
miundombinu yake kama kumbu za kisasa na mengineyo kama hayo.
Hadi sasa, hakuna kumbi
za kisasa za mchezo huo hapa nchini ambazo zingesaidia kuwahamasisha vijana
wadogo wa kitanzania kujikita katika ndondi.
Hatahivyo, bado kila
siku ya Mungu vijana wa kitanzania wameonekana ‘kupambana’ kujaribu kuendeleza
vipaji vyao kupitia ndondi, baadhi yao wakifanya hivyo bila kupata uangalizi
sahihi wa kitaalamu.
Mathalani, katika mitaa
mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, unaweza kuwakuta vijana wadogo wakiwa
wamening’iniza kiroba kilichojaa mchanga juu ya mti, wakijifua waweze kutimiza
ndoto zao za kuwa mabondia maarufu hapa nchini na duniani kwa ujumla.
Wapo wanaofanya hivyo
ili waweze kufikia mafanikio ya mabondia waliopita kama Yombayomba, Simba;
lakini wengi wakisikika wakimtaja Rashid Matumla, ambaye ndiye bondia wa miaka
ya hivi karibuni kuwahi kutamba hapa nchini na hata katika medani ya kimataifa,
akitwaa mikanda lukuki kabla ya kustaafu.
Yusuph Mnyate ‘Super
Boy’, ni miongoni mwa vijana wenye vipaji vya ndondi ambaye ameona ni vyema
akakitendea haki kipaji chake hicho.
Kijana huyo mwenyeji wa
mkoani Tanga, ni mwajiriwa wa Jeshi la Polisi chini ya Mkuu wa Jeshi la Polisi
Tanzania (IGP) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova, akiwa anapatikana pale Polisi Ufundi, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam,
ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya ndondi ya Polisi jijini.
Na baada ya kudumu katika ndondi za ridhaa kwa muda mrefu kidogo,
Mnyate ameamua kubadili upepo na kuhamia kwenye ndondi za kulipwa.
Akizungumzia uamuzi wake wa kuhamia ndondi za kulipwa, Mnyate anasema
kuwa alifanya hivyo kama sehemu ya hatua za maisha yake katika mchezo huo
aliodai kuwa anaupenda mno.
“Nimekuwa katika ngumi za ridhaa kwa muda mrefu, na sasa nimeamua
kuhamia ndondi za kulipwa, nikiamini ninaweza kupata mafanikio makubwa kwani
nina usongo wa kulipa sifa Jeshi la Polisi pamoja na nchi yangu kwa kufanya
mambo makubwa kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa.
“Katika maisha yangu ya ndondi, nimekuwa nikipata sapoti ya hali ya
juu kutoka kwa mwajiri wangu na wachezaji wenzangu ambao nao ni askari Polisi…
naondoka ngumi za ridhaa kwenda za kulipwa, nataka kurejesha hadhi ya ndondi
ndani ya Jeshi la Polisi.
“Matarajio yangu ni kufuata nyayo za Haji Matumla ambaye ni askari
Polisi, Yombayomba (Michael) na wenginbeo, ikiwezekana hata kuwazidi, naamini
hilo linawezekana kama kila kitu kitakwenda kama nilivyopanga.”
Aliongeza: “Nataka kufanya kitu tofauti, nashukuru hata rafiki na
ndugu zangu, wananisapoti, sitaki kubahatisha, ndio maana nimetafuta kocha
mzuri mwenye uzoefu, kama Rashind Matumla, ambaye nashukuru amenipokea na kunikaribisha
katika ‘gym’ yake.
“Kwangu Rashid Matumla ni mtu muhimu sana, nimekuwa nikimshabikia
tangu nilipokuwa mtoto na nilitamani siku moja nije kuwa kama yeye au hata
kumzidi.
“Kufanya mazoezi katika ‘gym’ yake (Matumla), kunanisisimua sana, ninapoona
picha zilizopo katika ukuta wa gym yake akiwa anapigana, akiwa amebeba mikanda
mbalimbali ya ubingwa wa Dunia, na hata habari za kwenye magazeti za
kumpongeza, ninapata hisia kali sana.”
Anasema kuwa kikubwa zaidi, ni kuona bingwa huyo wa zamani wa Dunia wa
WBU ambaye alishiriki mara tatu michezo ya Olimpiki, mwaka 1988, 1992 na 1996,
akimpa moyo wa kufuata nyayo zake
“Kaka Rashid amekuwa akinipa moyo kuwa kutokana na jinsi alivyoniona,
ninaweza kuwa bondia mzuri kama yeye au hata kumzidi, lakini kama nitafanya
bidii katika mazoezi, kuzingatia nidhamu na miiko ya mchezo huu wa ngumi.”
Mnyate anaelezea hali ya ndondi ilivyo ndani ya Jeshi la Polisi,
akisema: “Polisi kuna wachezaji wazuri sana, tatizo ni hamasa, hivyo nimeona ni
vyema nikawafungulia njia wenzangu kwani hakuna sababu yoyote ya kutofika mbali
katika mchezo huo, maana mwajiri wetu anajali sana michezo si kama katika sekta
nyingine.”
Kwa upande wa ndondi za ridhaa, anasema kuwa tatizo lililoko huko ni
uongozi wa chama husika kutokuwa na mikakati ya kuuendeleza mchezo huo.
“Katika ngumi za ridhaa hapa nchini, tatizo ni uongozi, pale kuna mtu
mmoja tu, Mashaga (Makore), jamaa anajitahidi sana kupambana, kama angepata
msaada, basi mambo yangekuwa mazuri zaidi,” anasema.
Na sasa Mnyate ni ‘hakuna kulala’, kila baada ya kumaliza majukumu
yake ya kikazi, hugeukia mazoezi ya ndondi katika gym ya Matumla na wakati
mwingine kwenda kwenye klabu nyingine za mazoezi.
Katika mazoezi yake hayo, wakati fulani amekuwa pia akinolewa na
Haruna Andrew ‘Ndimu Mkata Shombo’ ambaye naye ni bondia.
Matarajio yake kwa siku chache zijazo ni kupata pambano la kujipima
nguvu dhidi ya bondia atakayejitokeza kukabiliana naye.
“Kabla ya kupata pambano, niliona ni vyema nikajifua kwanza kwani kuna
kipindi nilisimama kufanya mazoezi, hivyo lazima niwe fiti kabla ya kupanda
ulingoni,” anasema.
Anasema kuwa matarajio yake mapema mwezi ujao atakuwa fiti tayari
kuonyesha ubabe na bondia yeyote atakayekubali kupigana naye.
Hata hivyo, alisema kuwa katika kufanikisha azma yake hiyo, hatasita
kuwa bega kwa bega na mwajiri wake ambaye ni Jeshi la Polisi kuhakikisha kipaji
chake hicho hakiathiri majukumu yake ambayo ndiyo yanayomwezesha kufanikisha
baadai ya mambo kuelekea mkakati wake wa kuwa bondia hatari hapa nchini.
“Pamoja na haya yote, ninaiheshimu sana kazi yangu kwani ndiyo
inayonifanya niwe na jeuri ya kutamba kutaka kufuata nyayo za akina Matumla,
bila Jeshi la Polisi, nisingekuwa kama nilivyo sasa,” anasema Mnyate.
Bondia Yusuph Mnyate, alizaliwa Februari 20, mwaka 1982 katika eneo la
Ngamiani, jijini Tanga, akiwa ni mtoto w asaba katika familia ya watoto saba wa
Mzee Mnyate.
Alianza masomo yake
katika Shule ya Msambweni, jijini humo na baadaye kujiunga na Chuo cha Ufundi
Stadi (VETA) mwaka 1995.
Mnyate ambaye kwa sasa hajaona,
lakini akiwa na mchumba anayetarajia kufunga naye ndoa muda si mrefu, alijiunga
na Jeshi la Polisi mwaka 2000 na hadi sasa analitumikia jeshi hilo, kwa umakini
na uadilifu wa hali ya juu.
Pamoja na kulitumikia
Jeshi la Polisi na kuendeleza kipoaji chake cha ndondi, Mnyate anekuwa akitenga
muda wake kwa ajilki ya kujiendeleza kimasomo.
“Kama unavyofahamu,
elimu ni kila kitu na haina mwisho, nashukuru mwajiri wangu (Jeshi la Polisi),
hana kikwazo na mtu anayetaka kujiendeleza kimasomo, kwa kweli ninashukuru sana
kwa hilo,” anasema Mnyate.
Juu ya mkakati wake wa
kuendelea na masomo, anasema: “Ndondi inaonekana kama ni mchezo wa akina
‘Kayumba’ (watu wasio wasomi), tusikubali ujinga, mabondia twendeni shule.”
Kuhusiana na malengo
yake baada ya kuanza kupata mafanikio katika ndondi, anasema amepania kufungua
klabu yake ya mazoezi ya ndondi (gym) ambayo itakuwa katika ubora wa hali ya
juu ili kuwawezesha vijana chipukizi kujinoa waweze kutimiza ndoto zao.
“Lengo langu ni kufungua ‘gym’ ambayo itakuwa na hadhi ya kimataifa,
kama ilivyo Azam Complex ya klabu ya soka ya Azam.
Juu ya kilio cha mabondia wengi kutaka wadhamini kujitokeza katika
mchezo huo, Mnyate anaasa: “Tusitegemee zaidi wadhamini, tujitegemee,
tusipigane kuganga njaa, kwani tunadhalilishwa kwa kutojitambua, maana ukipigwa
unajirudisha nyuma na umaarufu wako unapotea.”
MSETO tunamtakia kila la kheri Yusuph Mnyate kuelekea jitihada zake za
kuwa bondia wa kulipwa mwenye mafanikio hapa nchini, tukiamini hilo
linawezekana iwapo atajipanga hasa na kuzingatia miiko ya mchezo huo.
Kwa maoni, ushauri 0783324232
No comments:
Post a Comment