Naibu Waziri ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Kassim Majaliwa (wa pili kulia) akisalimiana na Meneja Biashara Idara ya Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Grace Lyon mara baada ya kuwasili kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutokomeza Fistula yaliyofanyika kitaifa katika Wilaya Mbogwe, Geita. Kulia ni Kaimu Mkuu wa wilaya ya Mbogwe, Amani Mwenegoha na Kushoto ni Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Haika Mawalla na wa pili kushoto ni Mwakilishi msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania, Dkt.Rutasha Dadi.(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog)
Na Zainul Mzige wa modewjiblog
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani(UNFPA) limekabidhi msaada wa gari la wagonjwa lenye thamani ya shilingi milioni 80 katika kituo cha afya cha Masumbwe kilichopo katika Wilaya mpya ya Mbogwe Mkoani Geita.
Shirika hilo limetoa vifaa vya kutoa huduma ya upasuaji vyenye thamani ya shilingi milioni 250 katika kituo hicho mbali na kutumia shilingi zaidi ya shilingi milioni 100 kusadia ujenzi wa jengo la upasuaji katika kituo hicho.
Misaada hiyo kwa pamoja ilikabidhiwa Jumamosi iliyopita katika halfa ambaye mgeni rasmi alikuwa ni Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Kassim Majaliwa.
Majaliwa alishuruku UNFPA kwa msaada huo na kutaka utumike vizuri ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
“ Nimeona vifaa vya hospitali vingi na vya gharama kubwa, sasa ni wajibu wetu kuvitunza na kuvitumia vizuri. Mfano gari tu limegharimu shilingi milioni 80. Huu ni msaada mkubwa sana na kwa niaba ya serikali nawashukuru sana UNPFA, tutaendelea kushirikiana”, alisema Majaliwa .
Hata hivyo Naibu Waziri huyo aliwaagiza vingozi wa Halmashuri ya Wilaya ya Mbogwe kuhakikisha kuwa gari hilo linatumika kusafirisha wagonjwa tu na sio vinginevyo.
Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Haika Mawalla (kushoto) na Mwakilishi msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania, Dkt.Rutasha Dadi wakipitia ratiba ya sherehe za maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutokomeza Fistula ambapo kitaifa yamefanyika katika Wilaya Mbogwe, Geita.
“ Gari hili litumike kwa matumizi ya wagonjwa tu. Sitegemei kusikia kuwa linapeleka wafanyakazi sokoni kununua nyanya. Na Mkurugenzi atenge bajeti ya mafuta ya gari hili muda wote”, aliagiza Majaliwa.
Hafla ya makabidhiano ya misaada hiyo ilienda sambamba na maadhimisho ya siku ya kutokomeza tatizo la ugonjwa wa Fistula duniani yaliyofanyakia kitaifa katika viwanja vya shule ya msingi Masumbwe katika Wilaya ya Mbogwe , Mkoani Geita.
Akizungumuza katika hafla hiyo Mwakilishi msaidizi wa Shirika la UNFPA, Dkt. Rutosha Dadi alisema msaada wa vifaa walivyotoa utasadia kumaliza tatizo la Fistula na kuboresha huduma zingine za afya .
“ Tumefanya ukarabati mkubwa sana katika jengo la upasuaji na kutoa vifaa vya kisasa kama vile Ultrasound”, alisema Dkt. Dadi.
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Mbogwe, Amani Mwenegoha (wa nne kulia) akitoa salamu na kumkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na umati wa wakazi wa Mbogwe waliokusanyika kwenye maadhimisho hayo. Kutoka kushoto ni Meneja wa miradi ya AMREF, kanda ya ziwa Dkt. Awene Gavyole, Makamu Afisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Bi. Haika Mawalla, Mwakilishi msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania, Dkt. Rutasha Dadi, Katibu Tawala wa mkoa wa Geita, Charles Palanjo, mgeni rasmi Naibu Waziri ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Kassim Majaliwa, Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita, Joseph Kisalla, Meneja Biashara Idara ya Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Grace Lyon pamoja na Mbunge wa jimbo la Mbogwe, Mh. Augustino Masele.