MD Digital

Wednesday, September 21, 2011

Mti wa Matunda unapochanwa Mbao

Wakazi waKipera wakichana mbao mti waMzambarau kijijini hapo.

KUNDI LA T-MOTO MODERN TAARAB LATUA DAR KUFYATUA SITA MPYA KWA MPIGO

KUNDI jipya la muziki wa taarab la Tanzania Moto Modern Taarab (T-Moto) limetua jijini Dar es Salaam leo asubuhi kutoka mfichoni katika Visiwa vya Zanzibar, lililokuwa limejichimbia kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi wake uliosogezwa mbele hadi Oktoba 28 mwaka huu.
Kundi hilo limewasili jijini baada ya kusitisha mazozi yake kwa muda kwa ajili ya maombolezo ya msiba wa Meli ya Mv Spice na linatarajia kuingia studio kwa ajili ya kurekodi nyimbo zake mbili kati ya zilizosalia ili kukamilisha albamu yao.
Akizungumza katika Bandari ya jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kundi hilo Amin Salmin, alisema kwamba kundi hilo litaingia katika stuio za Bakunde na kurekodi nyimbo sita ambazo zitakamilisha albamu yao iitwayo ‘Aliyeniumba Hajanikosea’.
Aidha alisema kuwa baada ya kumaliza zoezi la kurekodi nyimbo hizo, kundi hilo linatarajiwa kufanya ziara katika mikoa ya Tanzania na nchi jirani ya Kenya, kabla ya kufanya uzinduzi rasmi wa kundi na albamu yao Oktoba 28, jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wasanii wa kundi hilo ambaye ni mkongwe katika muziki huo wa Taarab, Bi. Mwanahawa Ally alisema anashukuru kambi hiyo imewaweka katika mwelekeo mzuri ambapo anaamini kazi zitakazotoka zitakuwa na viwango vya hali ya juu hivyo amewaomba mashabiki wakae mkao wa kula.
“Nataka niwaeleze mashabiki wa tasnia ya taarab kwamba tunakuja kwa moto kama lilivyo jina la kundi letu, moto ambao si rahisi kuzimika kwa kijipipa cha maji, hivyo mashabiki wetu wasubiri mambo mazuri na ya kupendeza kutoka kwetu, tunawaomba mashabiki watupokee vizuri kwa kujitokeza kwa wingi katika maonyesho yetu,”Alisema.
Tayari kundi hilo limeshatoa nyimbo mbili ambazo zimeweza kuliwatambulisha vyema.
Nyimbo hizo ni pamoja na uliobeba albamu hiyo‘ Aliyeniumba Hajanikosea’ ulioimbwa na Mwanahawa Ally, pamoja na ‘Unavyojidhani Mbona Hufanani’ ulioimbwa na Jokha Kassim.
Nyimbo nyingine zinazotarajiwa kuwamo katika albamu hiyo ni pamoja na ‘Mtoto wa Bongo’ ulioimbwa na Hassan Ally, ‘Mchimba Kaburi Sasa Zamu yake imefika’ ulioimbwa na Mrisho Rajab, ‘ Mwenye Kustiri Mungu’, ‘Kumbe Wewe ni Shoti’ ambazo zimeimbwa na Mosi Suleiman na ule wa ‘ Riziki na Shortcut’ ulioimbwa na Aisha Masanja.
Kundi hilo limesheheni wasanii wenye vipaji vya hali ya juu wakiwemo Mwanahawa Ally, Jokha KAssim, Jumanne Ulaya ‘Mkono wa Biashara’, Mrisho Rajab, Musa Mipango, Hassan Ally, Mosi Suleiman, Rajab Kondo, Fadhili Mnara, Moshi Mtambo, Ally Kabura, Sabha, Rahma , Asha Masanja na Hanifah Kasim na wengineo.