MD Digital

Sunday, March 17, 2024

MAKALA: WANANCHI KATA 22 WASIKILIZENI WAGOMBEA, MPIGE KURA

Wagombea wa vyama mbalimbali wakiangalia fomu za uteuzi wa wagombea walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugombea nafasi ya udiwani Kata ya Kimbiji iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Dar es Salaam. 
********"""
Na Mroki Mroki

TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Machi 20,2024 kuwa ni siku ya kupiga kura katika Uchaguzi Mdogo wa udiwani katika Kata 23 za Tanzania Bara.

 

Tume ilitangaza uchaguzi huo baada ya kuketi katika kikao chake cha Februari 15 mwaka huu na siku hiyohiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K  akatoa taarifa kwa umma juu ya uwepo wa uchaguzi huo mdogo.

 

Tayari mchakato wa Uchaguzi huo umeshaanza ambapo Februari 27 hadi Machi 4, 2024 wagombea walichukua fomu za uteuzi, uteuzi ulifanyika Machi 4,2024 na kampeni za uchaguzi zilianza Machi 5,2024 na zinaendelea hadi tarehe 19 Machi, 2024.

 

Hata hivyo, baada ya hatua ya uteuzi, Kata ya Nkokwa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ilipata mgombea mmoja tu aliyeteuliwa bila kupingwa hivyo hakutakuwa na kampeni kwenye Kata hiyo. Hivyo, uchaguzi utafanyika kwenye kata 22 zilizobakia.

 

Kata zitakazofanya uchaguzi huo mdogo ni Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Fukayosi(Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).

 

Nyingine ni  Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya  Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Mshikamano (Halmashauri ya Manispaa ya Musoma), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu) Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).

 

Katika Uchaguzi huu wa Kata 22, Vyama vya siasa 18 vimesimamisha wagombea 127 kati ya hao wanaume ni 89 na wanawake ni 38. Wagombea kutoka kwenye vyama hivyo walichukua fomu za uteuzi na kuzirejesha na hatimaye wakateuliwa kuwania nafasi hiyo.

 

Wagombea wa vyama mbalimbali wakiangalia fomu za uteuzi wa wagombea walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugombea nafasi ya udiwani Kata ya Kimbiji iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Dar es Salaam. 

Wagombea wote wameaminiwa na kupewa ridhaa na vyama vyao vya siasa kuwania nafasi zilizowazi,  kwa kufanya hivyo, vyama hivyo vya siasa  vimewatendea haki wanachama wao na wananchi kwa ujumla kwa kuwa wamepata haki ya kikatiba ya kugombea lakini pia wanachama na wananchi, watapata haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.

 

Wagombea walioteuliwa na Tume ni wale waliopendekezwa na vyama vyao vya siasa kugombea kiti cha udiwani ambapo pia walijaza na kuwasilisha fomu za uteuzi katika Ofisi za Uchguzi katika Kata husika.

 

Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata walisimamia vyema majukumu yao ya kutoa fomu za uteuzi. Fomu za uteuzi za wagombea wote ziliwasilishwa siku ya uteuzi kabla ya saa kumi kamili (10:00) jioni.

 

Wagombea hawa wote siku ya uteuzi walijaza na kusaini mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Fomu Na. 10 ya maadili ya uchaguzi.

 

Wagombea hawa walijaza fomu hizo   kukiri kuheshimu na kuyazingatia maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa na  viongozi wa vyama vyao mwaka 2020 wakati wa uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara.

 

Uwepo wa maadili ya Uchaguzi unalenga hasa kuwa na uchaguzi huru, wa haki, uwazi na wa kuaminika. Na kwamba amani, ustawi wa nchi, usalama wa raia, uhuru wa vyama vya siasa na utii wa sheria , kanuni na taratibu za uchaguzi ndio msingi wa uchaguzi ulio huru, haki na wenye kuzingatia ushiriki wa makundi yote ya jamii katika uchaguzi.

 

Vyama vya Siasa, Serikali na Tume walikubaliana kuwajibika kuyatekeleza Maadili hayo yanayotokana na kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343. Viongozi hao kwa pamoja walisema “Tutafanya jitihada za wazi kuhakikisha Maadili haya yanajulikana na kuheshimiwa na wagombea pamoja na wanachama wote wa vyama vya siasa”.

 

Sheria, Kanuni na miongozo yote iliyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 bado inatumika na kufuatwa na vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchagzi na Serikali katika chaguzi hizi ndogo za udiwani.

 

Tayari Kampeni za uchaguzi zimeanza tangu siku moja baada ya uteuzi na zitaendelea hadi siku moja kabla ya siku ya kupiga kura.

 

Wakati wote wa kampeni wagombea wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni za uchaguzi, Maadili ya Uchaguzi na ratiba za kampeni.

 

Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi na ratiba za kampeni utasaidia katika kuweka uwanja sawa katika kipindi chote cha kampeni na siku ya uchguzi.

 

Vyama vya Siasa na wagombea pamoja na wafuasi wao wanapaswa kuepuka kufanya siasa za fujo na za vitisho dhidi ya upande mwingine.

 

Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, imepewa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia taasisi au asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo.

 

Tume itatoa elimu kwa wananchi katika maeneo yote ambayo yanafanya uchaguzi mdogo. Lakini pia zipo asasi ambazo zimepewa kibali na Tume kutoa elimu hiyo kwa baadhi ya maeneo.

 

Elimu hiyo inayotolewa ni ile ya kumuwezesha Mpiga Kura kutambua sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ikiwa ni pamoja na utaratibu mzima wa kufunguliwa na kufungwa kwa vituo vya kupigia kura. 

 

Lakini pia elimu hiyo itasaidia kutoa hamasa kwa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba katika kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.

 

Ni muhimu wananchi katika maeneo yote yanayofanya uchaguzi mdogo wakajitokeza kwa wingi kusikiliza sera za vyama na wagombea kisha kwa utashi wao wachague viongozi wanaowafaa kujaza nafasi zilizowazi katika Kata 23 za Tanzania Bara.

 

Mwandishi wa Makala haya ni Afisa Habari Msaidizi Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Thursday, January 25, 2024

MTOTO AKAA ICU SIKU 60, HOSPITALI IKITUMIA MILIONI 10,100,000 KUMTIBU

 
Na Raymond Mtani-BMH          
Novemba 11, 2023, Bi. Janeth (35), mkazi wa Manyoni Singida, alifika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) baada ya kukaa siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni akiimuuguza mwanaye aliyepatwa “degedege”.
 
Siku hiyo, ikawa safari ya siku 60 za mtoto wake huyo mwenye umri wa miaka 4 kwenye Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda ya Kati.
 
“watu walikuwa wanakuja, wanaruhusiwa wanamuacha mwanangu, wakati mwingine anabaki peke yake”.  alisema Bi. Janeth.
 
Dkt. Venance Misago ni Bingwa wa Ganzi na Wagonjwa Mahututi, na Mkuu wa Idara ya Huduma za Uangalizi Maalumu BMH amesema, Moyo wa mtoto huyo ulisimama ghafla (cardiac arrest) mara nne (4) ndani ya siku 60 mtoto huyo alipokuwa ICU.
 
“aligundulika kuwa na maambukizi kwenye Ubongo (meningitis), hali iliyokuwa inasababisha apoteze fahamu mara kwa mara” alieleza Dkt. Misago.
 
Aidha, Dkt. Misago amesema kuwa kwa kawaida mgonjwa hukaa katika Chumba cha uangalizi maalumu siku 3 hadi 14 lakini maambukizi aliyokuwa nayo mtoto huyo yalisambaa kiasi cha kusababisha presha kushuka na kupelekea Moyo kusimama (septic shock) mara kwa mara.
 
Ingawa hali hiyo haikuwa rahisi kwa Bi. Janeth, hakusita kumshukuru Mungu, Madaktari na Wauguzi waliyomhudumia mwanaye.
 
“...nilipitia wakati mgumu kiasi cha kukata tamaa, namshukuru Mungu kwa kumponya mwanangu, nawashukuru Madaktari na wauguzi kwa kumpambania mwanangu” alieleza Bi. Janeth kwa furaha.
 
Kwa mujibu wa Awadhi Mohamed, Mkurugenzi Msaidizi huduma za Usitawi wa Jamii Hospitali ya Benjamin Mkapa imetumia Shilingi 10, 100,000 kugharamia dawa, vifaa tiba na chakula kwa kipindi chote cha siku 60 Mtoto wa Bi. Janeth alipokuwa ICU.
 
Kupona kwa mtoto huyo ni kielelezo cha faida za uwekezaji katika sekta ya Afya nchini, hasa mapinduzi yanayofanywa katika kuboresha huduma za Wagonjwa Mahututi.
 
Ingawa, wakosoaji wa serikali hasa Wizara ya Afya wamekuwa na jicho la kutoridhishwa na hatua za maboresho hususani kasi ya utekelezaji na ubora wa huduma, historia ni mwalimu mzuri.
 
Historia inakili kwamba, maboresho ya huduma ni mchakato, huduma za Afya nchini haziwezi kutokea ghafla mithili ya kimbunga, zinapitia mkondo huo huo wa mchakato wa maboresho ikiwa ni pamoja na huduma za ICU.
 
Mathalani, taarifa za Maktaba ya Historia ya Tiba ya Nchini Marekani zinadokeza mchakato wa maboresho ya huduma za ICU katika nchi za Ulaya ulianza kwa kanuni za kutenga majeruhi wa vita vya Crimean kwa kuwaweka mahututi jirani na vituo vya wauguzi (nursing stations) ili wapewe uangalizi maalumu.
 
Hiyo ilikuwa 1854, maboresho hayo yaliyohamasishwa na Bi. Florance Nightingale kusaidia kuokoa Maisha ya Majeruhi wengi wa vita, Ulaya ilisubiri karibu miaka 100 na mlipuko wa Polio kuwa na ICU ya kwanza, iliyojengwa 1953 huko Copenhagen, Denmark.
  
Hali hii ni tofauti na Tanzania, kwa mujibu wa Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, alipowasilisha Makadiliyo ya bajeti, mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, aliliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu hatua kubwa zilizopigwa katika huduma za Wagonjwa Mahututi.
 
Waziri huyo wa Sekta ya Afya, alinukuliwa Mei 12, 2023 akisema kuwa baada ya shambulio la Uviko 19, serikali imeweza kuongeza wodi za Wagonjwa Mahututi kutoka 45 had 258 ndani ya kipindi cha miaka 2, yaani 2020 hadi 2023.
 
“Tunaweza kulaza wagonjwa mahututi 1000 kila siku nchini” alisema Mhe. Ummy Mwalimu.
 
Hapana shaka, kama ilivyo kwa Mtoto wa Bi. Janeth, maboresho ya huduma za ICU yaliyofanyika katika kipindi hicho cha miaka 2 yamesaidia kuokoa maelfu ya Maisha ya Watoto na watu wazima waliyokumbwa na changamoto mbalimbali za kiafya zilizowalazimu kuhitaji ICU.
 
Mwaka 2020, Hospitali ya Benjamin Mkapa ilikuwa na Wodi ya Wagonjwa Mahututi yenye vitanda 6 pekee, lakini kupitia maboresho hayo, hadi Makala haya yanaandi.kwa, Hospitali hiyo ina Wodi mbili za wagonjwa Mahututi zenye vitanda 22.
 
Kwa mujibu wa Dkt. Misago, vitanda hivyo vina mashine za kusafisha mfumo wa hewa (Suction Machine), mashine za kusaidia kupumua (Ventilator), mashine za kusaidia Moyo, Figo na Kuzuia damu Kuganda (Syringe pump and Infusion Pump) pamoja na mashine za uangalizi wa mwenendo wa matibabu ya Mgonjwa (Monitors).
 
Hali hiyo, inasaidi kuokoa Maisha ya wanchi wengi wenye kuhitaji huduma hizo kwa uhakika, kumbuka iliichukua Ulaya miaka 99 kupata ICU ya kwanza, huku Tanzania ikijenga ICU zaidi ya 200 ndani ya siku 730.

Monday, October 2, 2023

MWENGE WA UHURU WARIDHISHWA UBORA WA MIRADI WILAYA YA IKUNGI

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili (kulia), akimkabidhi Mwenge wa Uhuru, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson baada ya kumaliza mbio zake za kukagua miradi katika wilaya hiyo, Septemba 25, 2023.

*************
Na Dotto Mwaibale, Ikungi
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim ameridhishwa na utekelezaji wa miradi yote illyopitiwa na kukaguliwa na Mwenge huo wilayani Ikungi mkoani Singida na kueleza kuwa imekamilishwa kwa viwango vya ubora wa hali ya juu ambao umeendana na thamani ya fedha.

Kaim akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo Septemba 26, 2023 ikiwa ni siku yake ya nne ya mbio za mwenge alisema miradi yote ipo vizuri na kuwa mapungufu madogo madogo yaliyopo aliomba yafanyiwe kazi haraka ili kuiboresha zaidi.

Kiongozi huyo aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kubuni chanzo kipya cha mapato ambacho ni stendi mpya ya mabasi iliyojengwa eneo la Unyahati kutokana na fedha za mapato ya ndani.

“Niwapongeze kwa ubunifu mkubwa mlioufanya kwa kuanzisha stendi hii ambayo itakuwa chanzo kikubwa cha mapato,” alisema Kaim.

Aidha, aliagiza uongozi wa halmashauri hiyo kujenga vizimba kwa ajili ya kuwekea taka pamoja na kupanda miti kuzunguka stendi hiyo ili iwe katika mandhari nzuri.

Kaim alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikileta fedha nyingi kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali hivyo ni jukumu la watendaji kuhakikisha wanaisimamia ili iwe inajengwa kwa viwango vya ubora ambavyo vinaendana na thamani ya fedha.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson akitoa  taarifa ya miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru alisema ni saba na ina thamani ya Sh.Bilioni 2.14 na program mbalimbali tano.

Alitaja baadhi ya miradi iliyotembelewa kuwa ni mradi wa maji uliopo Kijiji cha Matare Kata ya Unyahati ambao umegharamiwa na fedha za Benki ya Dunia kupitia programu ya pforR uliotengewa Sh.386,898,900 na mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu sita ya vyoo uliopo Shule ya Msingi ya Matare katika Kijiji cha Matare Kata ya Unyahati.

Alitaja miradi mingine kuwa ni Kitalu cha miti uliopo Kijiji cha Mungaa Kata ya Mungaa ambao tangu kuanzishwa kwake jumla ya miche 965,000 imezalishwa na kuwa unatekelezwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Anti-Desert- Environment Scheme (ADESE) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzani (TFS) na unafadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Trees for the Future lililopo mjini Singida.

Apson alitaja miradi mingine kuwa ni Kikundi cha kufyatua matofali Vijana Chapakazi Ikungi ambacho kilianzishwa Desemba 6, 2022 na kukopeshwa mkopo wa Sh.Milioni 25 na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi.

Alitaja programu zilizotembelewa na Mwenge huo kuwa ni ya mapambano dhidi ya Malaria na mapambano dhidi ya dawa za kulevya, damu salama, mapambano ya VVU, masuala ya lishe, mapambano dhidi ya rushwa na Ukimwi na usafi wa mazingira. 

Apson alisema Mwenge huo umekimbizwa umbali wa kilometa 137.7.ukifanya shughuli za uwekaji wa jiwe la msingi, uzinduzi na kutembelea miradi hiyo saba na kuwa kauli mbiu ya mbio hizo za Mwenge wa Uhuru 2023 ni Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi.

Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)_Nusrat Hanje alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Kwa dhati kabisa ya moyo wangu niipongeze Serikali ya  Rais Dk. Samia kwa kutuwezesha sisi watu wa Mkoa wa Singida na nimpongeze kaka yangu Mbunge Miraji Mtaturu kwa kusimamia vizuri miradi inayoletwa na kuhakikisha inakamilika kwa thamani ya fedha zilizotolewa,” alisema Hanje.

Akitoa salamu Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe naye aliungana na viongozi wenzake akiwepo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi, Mika Likapakapa kumshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya na kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ambapo aliwaomba wananchi ilipo miradi hiyo kutunza miundombinu yake.

Kesho Septemba 27 timu nzima ya wakimbiza Mwenge huo wakiongozwa na Kiongozi wao wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, Abdalla Shaib Kaim watatembea na kukagua miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Itigi.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson  akimkabidhi Risala ya Utii Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim ili akamkabidhi Rais Samia Suluhu Hassan.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Rashid Rashid akiwa ameushika mwenge huo kabla ya kuanza kukimbizwa wilayani humo.
Vijana wa Skauti Khalid Abdallah (kushoto) na Mafongwe Tenga wakimvika Skafu Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 wakati wakimkarisha Iilaya ya Ikungi kuanza kukimbiza mwenge huo.
Vijana wa Skauti wakimvika Skafu Mkimbiza mbio za Mwenge wa Uhuru, Atupokigwe Elia kutoka Dodoma wakati wakimkarisha Iilaya ya Ikungi kuanza kukimbiza mwenge huo

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim, akipanda mche wa mparachichi katika viwanja vya Shule ya Msingi Matare ikiwa ni kuhifadhi mazingira.


Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim akipata maelezo kutoka kwa Mtaalam wa masuala ya Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim, akionesha umahiri wa kupika mboga za majani alipotembelea banda la Lishe katika Shule ya Msingi Matare.
Vijana wa Skauti wakiwa tayari kwa mapokezi ya wakimbiza Mwenge wa uhuru 2023 eneo la Njiapanda barabara ya Arusha na Makiungu.
Vijana wa hamasa wakionesha umahiri wa kucheza sarakasi wakati wa mapokezi hayo.
Vijana wa Skauti wakionesha ukakamavu.
Vijana wa Skauti wakiwa kwenye mapokezi hayo.
Wajumbe wa kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya ya Ikunghi. wakionesha ukakamavu wakati wa mapokezi hayo.
      Wakimbiza mwenge wa Uhuru 2023 Wilaya ya Ikungi wakiwa tayari kwa kazi hiyo. Kutoka kushoto ni Ibrahim Njoka, Patrick Mande, Lucia Silvester, Paskali Charles, Jacob Mgwama na Rebeca Julius.,    
Shamrashamra za mapokezi hayo zikiendelea.
Viongozi wa Wilaya ya Ikungi wakionesha furaha zao wakati wa mapokezi wa mwenge huo.
Viongozi wa Wilaya ya Ikungi na Manispaa ya Singida wakifurahi pamoja wakati wa mapokezi hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Singida, Jeshi Lupembe akionesha furaha yake wakati wa mapokezi hayo.

Mstahiki Meya wa wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu naye akionesha furaha yake wakati wa mapokezi hayo.

Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Nusrat Hanje akimshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wana Singida na Taifa kwa ujumla.

Wakimbiza Mwenge wa Uhuru 2023 wakiwa tayari kupokelewa Wilaya ya Ikungi baada ya kumaliza mbio zao Manispaa ya Singida.
Mkufunzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Meja Musa Ngomambo, akizungumza wakati akiwaaga wananchi wa Manispaa ya Singida tayari kwa kukimbiza mwenge huo Wilaya ya Ikungi.
Viongozi wa Wilaya ya Ikungi wakionesha tabasamu wakati wa kupokea mwenge huo. Kutoka kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Rashid Rashid, Mkuu wa Polisi Mrakibu wa Polisi (OCD)_ Suzana Kidiku.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim, akizungumza wakati akiwaaga viongozi wa Manispaa ya Singida.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson, akimkabidhi mafuta ya alizeti Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim.
Umati wa watu ukiwa katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru eneo la Njia Panda 
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Makiungu wakiwa katika mapokezi ya Mwenge wakati wa ukaguzi wa mradi wa kitalu cha miti .uliopo Kijiji cha Mungaa Kata ya Mungaa
Muonekano wa kitalu hicho cha miti.
Mkimbiza Mwenge wa Uhuru 2023, Emmanuel Hondi kutoka Babati Mkoa wa Manyara, akikabidhiwa taarifa ya mradi wa kitalu hicho cha miti.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mungaa  wakati katika mapokezi ya mwenge huo.
Mapokezi ya mwenge huo yakiendelea.
Taswira ya mapokezi ya Mwenge huo Puma ambapo ulitembea na kukagua programu mbalimbali.
Mratibu wa Programu ya Malaria Wilaya ya Ikungi, Isaya Mawazo akitoa taarifa ya mapambano dhini ya malaria. kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim.akigawa vyandarua vilivyotolewa na Bohari ya Dawa (MSD) kwa ajili ya mapambano dhidi ya malaria.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim. akipata maelezo ya mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa alipotembea banda la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) willayani humo._
Mashujaa wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA)_ wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mkoa, Shujaa Dismas Kombe nao walikuwepo kwenye mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2023 eneo la Puma. 
Madiwani na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye mapokezi ya mwenge huo Stendi ya zamani ya mabasi ya wilaya hiyo ambapo mkesha wa mwenge ulifanyika. Wa pili waliokaa mbele kutoka kushoto ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Abubakar Muna.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim.akipata maelezo ya mapambano ya kudhibiti dawa za kulenya.
Programu ya usafi na utunzaji wa mazingira ikifanyika.
Vijana wa Kikundi cha kufyatua matofali Vijana Chapakazi Ikungi wakiwa katika mapokezi ya mwenge huo wakati ulipofika kukagua kikundi hicho.
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Mwanahamisi Omari (Aliyevaa kofia)_ akijibu kwa ufasaha maswali aliyokuwa akiulizwa na kiongozi wa mbio za mwenge baada ya kumsomea taarifa ya mradi huo.
Askari wa Jeshi la Akiba wakihimarisha ulinzi wakati Mwenge wa Uhuru 2023 ulipowasili Stendi ya Mabasi ya zamani ya wilaya hiyo ambapo ulikesha.
Wakimba mwenge wa uhuru wakipitia nyaraka mbalimbali za ujenzi wa Stendi mpya ya Mabasi ya Wilaya ya Ikungi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi, Mika Likapakapa akitoa salamu za chama wakati wa mapokezi hayo. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu. 
Chifu Thomas Mgonto (kulia) kutoka Siuyu wilayani humo akizungumza na Vijana kuhusu kuzingatia maadili. 
Uwekaji wa jiwe la msingi la Stendi Mpya ya Mabasi Wilaya ya Ikungi ukifanyika.
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Ikungi Mhandisi Hope Lihundi  akitoa maelezo ya mradi wa maji wa Kata ya Matare kwa Kiongozi wa mbio za mwenge kabla hajauzindua mradi huo.

Kiongozi wa mbio za mwenge Abdalla Shaib Kaim akimuhoji Mhandisi wakati akikagua miundombinu ya ujenzi wa Shule ya Msingi Matare.
Ukaguzi wa madawati na meza zake ukifanyika katika shule hiyo
Muonekano wa moja ya darasa lililojengwa kwenye shule hiyo.