MD Digital

Sunday, March 9, 2014

Mnyate ‘Super Boy’ ‘Mtoto’ wa Kova aliyepania kufuata nyayo za Matumla

Na Michael Komba
NDONDI ni miongoni mwa michezo ambayo imewahi kuitangaza vilivyo Tanzania katika anga ya kimataifa, kama ilivyokuwa kwa riadha.

Mabondia ambao waliwahi kuipeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, ni Michael Yombayomba, Habibu Kinyogori, Titus Simba, Emmanuel Mlundwa, Rashid Matumla na wengineo.

Soka ambayo ndio mchezo unaopendwa na kupewa kipaumbele zaidi hapa nchini, haujawahi kuiletea Tanzania mafanikio yoyote, zaidi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria.

Zaidi ya mafanikio hayo, timu yetu ya Taifa, Taifa Stars na hata klabu zetu, zimebaki kuwa ‘kichwa cha mwendawazimu’ katika michuano mbalimbali ya kimataifa.

Angalau riadha na ndondi zimefurukuta kwa kutwaa medali katika mashindano makubwa kama michezo ya Olimpiki na Michezo ya Afrika (All Africa Games’.

Pamoja na hilo, mchezo wa ndondi bado unaonekana kupewa kisogo na wadau kwa kushindwa kuboresha miundombinu yake kama kumbu za kisasa na mengineyo kama hayo.

Hadi sasa, hakuna kumbi za kisasa za mchezo huo hapa nchini ambazo zingesaidia kuwahamasisha vijana wadogo wa kitanzania kujikita katika ndondi.

Hatahivyo, bado kila siku ya Mungu vijana wa kitanzania wameonekana ‘kupambana’ kujaribu kuendeleza vipaji vyao kupitia ndondi, baadhi yao wakifanya hivyo bila kupata uangalizi sahihi wa kitaalamu.

Mathalani, katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, unaweza kuwakuta vijana wadogo wakiwa wamening’iniza kiroba kilichojaa mchanga juu ya mti, wakijifua waweze kutimiza ndoto zao za kuwa mabondia maarufu hapa nchini na duniani kwa ujumla.

Wapo wanaofanya hivyo ili waweze kufikia mafanikio ya mabondia waliopita kama Yombayomba, Simba; lakini wengi wakisikika wakimtaja Rashid Matumla, ambaye ndiye bondia wa miaka ya hivi karibuni kuwahi kutamba hapa nchini na hata katika medani ya kimataifa, akitwaa mikanda lukuki kabla ya kustaafu.

Yusuph Mnyate ‘Super Boy’, ni miongoni mwa vijana wenye vipaji vya ndondi ambaye ameona ni vyema akakitendea haki kipaji chake hicho.

Kijana huyo mwenyeji wa mkoani Tanga, ni mwajiriwa wa Jeshi la Polisi chini ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akiwa anapatikana pale Polisi Ufundi, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam, ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya ndondi ya Polisi jijini.

Na baada ya kudumu katika ndondi za ridhaa kwa muda mrefu kidogo, Mnyate ameamua kubadili upepo na kuhamia kwenye ndondi za kulipwa.
Akizungumzia uamuzi wake wa kuhamia ndondi za kulipwa, Mnyate anasema kuwa alifanya hivyo kama sehemu ya hatua za maisha yake katika mchezo huo aliodai kuwa anaupenda mno.

“Nimekuwa katika ngumi za ridhaa kwa muda mrefu, na sasa nimeamua kuhamia ndondi za kulipwa, nikiamini ninaweza kupata mafanikio makubwa kwani nina usongo wa kulipa sifa Jeshi la Polisi pamoja na nchi yangu kwa kufanya mambo makubwa kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa.

“Katika maisha yangu ya ndondi, nimekuwa nikipata sapoti ya hali ya juu kutoka kwa mwajiri wangu na wachezaji wenzangu ambao nao ni askari Polisi… naondoka ngumi za ridhaa kwenda za kulipwa, nataka kurejesha hadhi ya ndondi ndani ya Jeshi la Polisi.
“Matarajio yangu ni kufuata nyayo za Haji Matumla ambaye ni askari Polisi, Yombayomba (Michael) na wenginbeo, ikiwezekana hata kuwazidi, naamini hilo linawezekana kama kila kitu kitakwenda kama nilivyopanga.”
Aliongeza: “Nataka kufanya kitu tofauti, nashukuru hata rafiki na ndugu zangu, wananisapoti, sitaki kubahatisha, ndio maana nimetafuta kocha mzuri mwenye uzoefu, kama Rashind Matumla, ambaye nashukuru amenipokea na kunikaribisha katika ‘gym’ yake.
“Kwangu Rashid Matumla ni mtu muhimu sana, nimekuwa nikimshabikia tangu nilipokuwa mtoto na nilitamani siku moja nije kuwa kama yeye au hata kumzidi.
“Kufanya mazoezi katika ‘gym’ yake (Matumla), kunanisisimua sana, ninapoona picha zilizopo katika ukuta wa gym yake akiwa anapigana, akiwa amebeba mikanda mbalimbali ya ubingwa wa Dunia, na hata habari za kwenye magazeti za kumpongeza, ninapata hisia kali sana.”

Anasema kuwa kikubwa zaidi, ni kuona bingwa huyo wa zamani wa Dunia wa WBU ambaye alishiriki mara tatu michezo ya Olimpiki, mwaka 1988, 1992 na 1996, akimpa moyo wa kufuata nyayo zake 

“Kaka Rashid amekuwa akinipa moyo kuwa kutokana na jinsi alivyoniona, ninaweza kuwa bondia mzuri kama yeye au hata kumzidi, lakini kama nitafanya bidii katika mazoezi, kuzingatia nidhamu na miiko ya mchezo huu wa ngumi.”

Mnyate anaelezea hali ya ndondi ilivyo ndani ya Jeshi la Polisi, akisema: “Polisi kuna wachezaji wazuri sana, tatizo ni hamasa, hivyo nimeona ni vyema nikawafungulia njia wenzangu kwani hakuna sababu yoyote ya kutofika mbali katika mchezo huo, maana mwajiri wetu anajali sana michezo si kama katika sekta nyingine.”

Kwa upande wa ndondi za ridhaa, anasema kuwa tatizo lililoko huko ni uongozi wa chama husika kutokuwa na mikakati ya kuuendeleza mchezo huo.

“Katika ngumi za ridhaa hapa nchini, tatizo ni uongozi, pale kuna mtu mmoja tu, Mashaga (Makore), jamaa anajitahidi sana kupambana, kama angepata msaada, basi mambo yangekuwa mazuri zaidi,” anasema.

Na sasa Mnyate ni ‘hakuna kulala’, kila baada ya kumaliza majukumu yake ya kikazi, hugeukia mazoezi ya ndondi katika gym ya Matumla na wakati mwingine kwenda kwenye klabu nyingine za mazoezi.

Katika mazoezi yake hayo, wakati fulani amekuwa pia akinolewa na Haruna Andrew ‘Ndimu Mkata Shombo’ ambaye naye ni bondia.

Matarajio yake kwa siku chache zijazo ni kupata pambano la kujipima nguvu dhidi ya bondia atakayejitokeza kukabiliana naye.

“Kabla ya kupata pambano, niliona ni vyema nikajifua kwanza kwani kuna kipindi nilisimama kufanya mazoezi, hivyo lazima niwe fiti kabla ya kupanda ulingoni,” anasema.

Anasema kuwa matarajio yake mapema mwezi ujao atakuwa fiti tayari kuonyesha ubabe na bondia yeyote atakayekubali kupigana naye.

Hata hivyo, alisema kuwa katika kufanikisha azma yake hiyo, hatasita kuwa bega kwa bega na mwajiri wake ambaye ni Jeshi la Polisi kuhakikisha kipaji chake hicho hakiathiri majukumu yake ambayo ndiyo yanayomwezesha kufanikisha baadai ya mambo kuelekea mkakati wake wa kuwa bondia hatari hapa nchini.

“Pamoja na haya yote, ninaiheshimu sana kazi yangu kwani ndiyo inayonifanya niwe na jeuri ya kutamba kutaka kufuata nyayo za akina Matumla, bila Jeshi la Polisi, nisingekuwa kama nilivyo sasa,” anasema Mnyate.

Bondia Yusuph Mnyate, alizaliwa Februari 20, mwaka 1982 katika eneo la Ngamiani, jijini Tanga, akiwa ni mtoto w asaba katika familia ya watoto saba wa Mzee Mnyate.

Alianza masomo yake katika Shule ya Msambweni, jijini humo na baadaye kujiunga na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mwaka 1995.

Mnyate ambaye kwa sasa hajaona, lakini akiwa na mchumba anayetarajia kufunga naye ndoa muda si mrefu, alijiunga na Jeshi la Polisi mwaka 2000 na hadi sasa analitumikia jeshi hilo, kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.
Pamoja na kulitumikia Jeshi la Polisi na kuendeleza kipoaji chake cha ndondi, Mnyate anekuwa akitenga muda wake kwa ajilki ya kujiendeleza kimasomo.

“Kama unavyofahamu, elimu ni kila kitu na haina mwisho, nashukuru mwajiri wangu (Jeshi la Polisi), hana kikwazo na mtu anayetaka kujiendeleza kimasomo, kwa kweli ninashukuru sana kwa hilo,” anasema Mnyate.

Juu ya mkakati wake wa kuendelea na masomo, anasema: “Ndondi inaonekana kama ni mchezo wa akina ‘Kayumba’ (watu wasio wasomi), tusikubali ujinga, mabondia twendeni shule.”

Kuhusiana na malengo yake baada ya kuanza kupata mafanikio katika ndondi, anasema amepania kufungua klabu yake ya mazoezi ya ndondi (gym) ambayo itakuwa katika ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha vijana chipukizi kujinoa waweze kutimiza ndoto zao.

“Lengo langu ni kufungua ‘gym’ ambayo itakuwa na hadhi ya kimataifa, kama ilivyo Azam Complex ya klabu ya soka ya Azam.

Juu ya kilio cha mabondia wengi kutaka wadhamini kujitokeza katika mchezo huo, Mnyate anaasa: “Tusitegemee zaidi wadhamini, tujitegemee, tusipigane kuganga njaa, kwani tunadhalilishwa kwa kutojitambua, maana ukipigwa unajirudisha nyuma na umaarufu wako unapotea.”

MSETO tunamtakia kila la kheri Yusuph Mnyate kuelekea jitihada zake za kuwa bondia wa kulipwa mwenye mafanikio hapa nchini, tukiamini hilo linawezekana iwapo atajipanga hasa na kuzingatia miiko ya mchezo huo.

Kwa maoni, ushauri 0783324232

Wednesday, February 19, 2014

MATOKEO YA TATHMINI YA MCHAKATO WA UHAMAJI KUTOKA MFUMO WA UTANAGAZAJI WA ANALOJIA KWENDA KIDIJITI



1.0        UTANGULIZI 
 Mnamo mwezi Julai, 2013, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikamisheni jopo la wataalamu wa Chuo Kikuu kufanya tathmini ya mchakato mzima wa uhamaji toka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda mfumo wa kidijiti pamoja na uzimaji wa mitambo hiyo kwenye miji saba ambayo ni Dar e salaam, Tanga, Moshi, Mwanza, Dodoma, Arusha na Mbeya. Uzimaji wa mitambo ya analojia ilikuwa ni kwa mujibu wa sheria, ambayo iko kwenye kanuni zinazojulikana kama “Digital Broadcasting and Other Networks 2011”

Jopo hilo lilijumuisha wataalamu wafuatao:-

Prof. Nerey Mvungi         Mtaalamu wa Mawasiliano ya ki electronic
Dr.Francis Sichona         Mtaalamu wa Takwimu
Mr.F.M Ishengoma        Mtaalamu wa Habari na Mawasiliano

Wote hawa ni wafanayakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


1.1                MADHUMUNI YA TATHMINI
Madhumuni ya tahmini hii ilikuwa imejengwa kwenye maeneo Makuu manne kama ifuatavyo;

(a)  Tathmini ya utendaji na utoaji huduma za utangazaji kwenye mfumo wa kidijiti ikiwa ni pamoja na usimikaji wa miundo mbinu ya kidijiti.

(b) Tathmini ya kuangalia jinsi Mamlaka ya Mawasiliano ilivyokuwa imejizatiti kuandaa na kusimamia zoezi zima la uhamaji toka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda kidijiti

(c)  Tathmini ya jinsi watumiaji wa huduma za utangazaji walivyopokea mabadiliko hayo na changamoto zilizopo na

(d) Tathmini ya jinsi zoezi zima la uzimaji mitambo lilivyoendeshwa.

Katika uendeshaji wa tathmini hiyo wataalamu walizingatia mambo muhimu yafuatayo ikiwa ni pamoja na hoja zilizotolewa na taasisi na watu mbalimbali kutoka kwenye jamii kama ifuatavyo:-

(i)     Idadi ya visimbuzi vilivyokuwepo kwenye soko kabla ya uzimaji mitambo kama vinatosheleza mahitaji,

(ii)    Idadi ya watu walioweza kununua visimbuzi ilikuwa ndogo hivyo watu wengi kushindwa kununua na kukosa habari zinazopatikana kwa njia ya luninga,

(iii)  Ushirikishaji wa wadau kwenye mchakato mzima wa uhamaji toka mfumo wa analojia kwenda kidijiti kabla ya uzimaji mitambo hiyo,

(iv)  Kiwango cha Elimu kwa Umma (Public Awareness Campaign) kilichotolewa kabla na baada ya uzimaji mitambo,

(v)    Bei za visimbuzi kama zilikuwa juu kwa watu wa hali ya kawaida na kusababisha kushindwa kuvinunua,

(vi)  Ubora wa visimbuzi na upokeaji wa matangazo usioridhisha kama vile kuganda kwa picha.


1.2                NJIA ILIYOTUMIKA KUFANYA TATHMINI
Njia iliyotumika kufanya tathmini hii ni ile inayotumika kimataifa (International Best Practise) kuendesha mazoezi kama haya ijulikanayo kama “Sampling Approach” ambapo takwimu hukusanywa kwa kuzingatia uwiano wa kaya zilizopo kwenye eneo husika, jinsia, umri, elimu na kazi za kumuingizia kipato mtu anayehojiwa.

Makundi mabalimbali yanayohusika kwenye mchakato huu wa uhamaji kutoka mfumo wa analojia kwenda dijitali yalihojiwa kwa kupitia dodoso maalumu lililoandaliwa na maoni yao yalikusanywa. Makundi hayo ni kama ifuatavyo:-
(i)           Watumiaji wa huduma ya matangazo kwa mfumo wa kidijiti (Consumers)

(ii)          Watengenezaji na wasambazaji wa maudhui kwa njia ya Luninga (Content Service Providers)

(iii)        Wasimikaji wa miundo mbinu ya kidijiti (Multiplex Operators) na

(iv)        Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

2.0        MATOKEO YA TATHMINI
Yafuatayo ni matokeo ya zoezi zima la tathmini hiyo kama ilivyoendeshwa kwenye maeneo tajwa hapo juu.

2.1         TATHMINI YA UTENDAJI NA UTOAJI HUDUMA ZA UTANGAZAJI KWENYE MFUMO WA KIDIJITI IKIWA NI PAMOJA NA USIMIKAJI WA MIUNDO MBINU YA KIDIJTI.
Tathmini iliyoendeshwa na jopo la wataalam kuhusu utendaji na huduma kwa walaji kwa ujumla wake zimeonyesha yafuatayo;

(a)   Asilimia 89% ya kaya za watumiaji (consumers) walikuwa wakitumia huduma ya matangazo kwa mfumo wa kidijiti mara baada ya uzimaji wa mitambo ya analojia kwenye miji saba ambayo tathmini ilikuwa ikifanyika

(b)   Asilimia 11% ya kaya za watumiaji hawakuweza kupokea matangazo ya kidijiti kwa sababu mbalimbali kama ifuatavyo:-

-       5.5% hawakununua visimbuizi

-       0.1% ya Kaya, walisema visimbuzi vilikuwa havipatikani

-    3.2% ya Kaya, walishindwa kunua visimbuzi sababu ya bei kuwa juu

-       0.2% ya Kaya visimbuzi vyao vilikuwa vibovu

-     0.3% ya Kaya, visimbuzi havikuweza kupokea matangazo ya kidijiti kwa sababu ya mawimbi hayapatikani kwa ubora zaidi (Poor signal reception)

-       0.9% ya Kaya Luninga (TV screen) zilikuwa mbovu

-       0.7% ya Kaya hawakuwa na umeme
2.2        UTAYARI WA MAMLAKA YA MAWASILIANO KUANDAA NA KUSIMAMIA ZOEZI ZIMA LA UHAMAJI TOKA UTANGAZAJI WA MFUMO WA ANALOJIA KWENDA KIDIJITI

Jopo la wataalamu lililokuwa likiendesha tathmini hii liliweza kuthibitisha kuwepo kwa mambo yafuatayo pamoja na baadhi ya nyaraka kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA):-

-       Kuwepo kwa kamati ya Kiufundi inayoundwa na wadau mbalimbali ikiwa na kazi ya kutoa ushauri wa kiufundi kwa maswala yote yanayohusu uhamaji toka utangazaji wa analojia kweda kidijiti,

-       Kuwepo kwa dira madhubuti inayoonyesha mambo muhimu ya kutekelezwa kuelekea uzimaji wa mitambo ya analojia,

-       Kuwepo kwa sheria na kanuni zinazosimamia zoezi la uhamaji toka analoja kwenda kidijiti,

-       Kuwepo kwa nyaraka mbalimbali zinazoonyesha muhtasari wa vikao mbalimbali vilivyofanywa kati ya wadau na Mamlaka ya Mawasiliano.

              Vilevile Jopo la wataalamu liliweza kuthibitisha mambo yafuatayo:-

-    Muundo bora wa leseni unaozingatia utoaji huduma za matangazo ya kidijiti,

-    Utaratibu mzuri wa ushindani kwa njia ya wazi uliotumika kuwapata “Multiplex Operators” (wajenga Miundombinu na Wsambazaji wa matangazo),

-     Waraka unaonyesha mchakato wa namna ya kupata malipo yananayotakiwa kulipwa na watengenezaji na wasambazaji wa  maudhui (Transmission fee) kwa wenye leseni ya miundo mbinu ya kidijiti (Multiplex Operators),

-    Mfano wa nyaraka itakayotumika kufikia makubaliano ya utoaji huduma na mahusiano yao kibiashara (SLA) kati ya wasimikaji wa miundo mbinu ya kidijiti na watengenezaji na wasambazaji maudhui.

Kutokana na vielelezo na nyaraka ambazo jopo la wataalamu iliweza kuzipata, jopo limeridhika kabisa kuwa Mamlaka ya Mawasiliano ilikuwa imejizatiti vizuri kuandaa na kusimamia utekelezaji wa uhamaji toka mfumo wa zamani wa analojia kwenda utangazaji wa mfumo mpya wa kidijiti.

2.3          MATOKEO YA TATHMINI KUHUSU UPATIKANAJI WA VISIMBUZI NA ELIMU KWA UMMA

Tathmini imeonyesha kuwa kati ya kaya zote zilizohojiwa kwenye miji saba, ni 0.1% ya kaya zilizodai uhaba wa visimbuzi wakati wa zoezi zima la uzimaji mitambo ya analojia. Matokeo mingine ni kama ifuatavyo:-

-     35.4% ya kaya zilizohojiwa walinunua visimbuzi kabla ya uzimaji mitambo ya analojia na kabla ya kuanza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu mfumo mpya wa uatangazaji wa kidijiti

-    29.5% ya kaya walinunua visimbuzi kabla ya uzimaji mitambo ya analojia lakini baada ya utoaji elimu kwa umma

-       35.1% walinunua visimbuzi baada ya uzimaji mitambo
          Takwimu hizi zinaonyesha kuwa upatikanaji wa visimbuzi na bei halikuwa   tatizo kubwa lililoathiri mchakato mzima wa uhamaji kutoka mfumo wa      analojia kwenda kidijiti kwenye miji hii saba. Vilevile elimu kwa umma ilisaidia sana kuhamasisha walaji kuhamia kwenye mfumo huu mpya wa utangazaji


2.4           ZOEZI LA UZIMAJI MITAMBO YA ANALOJIA
Ilifahamika kuwa zoezi la uzimaji mitambo ya analojia lilifanyika kwenye awamu nne ambapo kila awamu ilitoa nafasi ya mwezi mmoja. Jopo la wataalam limeridhika na utaratibu huu, ambao unatoa nafasi kubwa ya kutathmini matatizo yanayojitokeza kwenye awamu ya kwanza kabla ya kwenda kwenye awamu nyingine. Vilevile ulitoa fursa ya kuhakikisha kuwa eneo linalofuata linakuwa na visimbuzi vya kutosha na elimu kwa umma inatolewa kikamilifu kwa kutumia Radio na Televissheni za eneo husika.


2.5          WATENGENEZAJI NA WASAMBAZAJI MAUDHUI (CONTENT SERVICE PROVIDERS)
65% ya watengenezaji na wasambazaji wa maudhui walikuwa wamejiunga na mfumo wa kidijiti kabla ya uzimaji wa mitambo ya analojia.
Sababu kubwa ya vituo vingine kutojiunga na mfumo huu kwa wakati ilikuwa ni sababu za kimazoea kwamba huenda mitambo isingezimwa kwa wakati uliopangwa.

Mpaka sasa vituo vyote vilivyopo Dar es Salaam vimeshajiunga na mfumo huu kasoro kituo kimoja.


3.0        MAJUMUISHO

3.1       Jopo la wataalam limeridhika kuwa watazamaji wengi waliokuwa kwenye mfumo wa analojia walijiunga kwenye mfumo wa kidijiti. 11% tu ndio ambao hawakuweza kujiunga kwa sababu mbalimbali kama nilizoelezea mwanzoni. Idadi hiyo inaweza kuwa imepungua kwa vile watu wamekua wakiendelea kununua visimbuzi,

3.2       Zoezi hili halijawanyima watanzania haki ya kupata habari kwani wengi tayari wameshajiunga na mfumo huu mpya. Jopo liliona kuwa sababu ya malalamiko mengi yalitokana na tabia halisi ya wanadamu kuogopa mabadiliko,

3.3       Kutokana na takwimu zilizokusanywa, jopo limeridhika kabisa kuwa elimu kwa umma ilitolewa kwa kiwango kikubwa kwani 90% ya kaya zilizotembelewa walikuwa na habari kuhusu mfumo huu mpya wa utangazaji kwa njia ya kidijiti,

3.4       Hatua madhubuti zilichukuliwa kuhakikisha kuwa kabla eneo husika kuzimwa mitambo ya analojia kulikuwa na visimbuzi vya kutosha,

3.5       Mfumo huu mpya wa kidijiti utatoa fursa nzuri kwa watengenezaji na wasambazaji wa maudhui kutumia muda wote kutengeneza vipindi vizuri badala ya kujihusisha na usimikaji miundo mbinu ya utangazaji,

3.6       Mfumo huu mpya wa utanagazaji kwa njia ya kidijiti umeongeza ubora wa picha na channel nyingi. Juhudi zifanyike kuwa na channel nyingi za nyumbani badala ya nje ya nchi.

3.7       Jopo limeridhika kuwa mfumo huu mpya haujapunguza idadi ya watazamaji wa luninga ila watazamaji wamegawanyika kutazama channel mbalimbali na hivyo kujenga hisia kuwa watazamaji wamepungua.

3.8       Maeneo mengi yaliyokuwa yanapokea channel moja mpaka tatu sasa wanaweza kuona channel za kinyumbani zaidi ya tano.

3.9       Uhamaji kutoka DVB-T kwenda DVB-T2 uende kwa nguvu ya soko kwani dhana nzima ilikuwa kuhama mfumo wa analojia kwenda kidijiti, na viwango vyote hivi viwili vinatoa matanagazo ya kidjiti


4.0        HITIMISHO

Kutokana na matokeo ya tathmini iliyofanyika serikali inashauriwa iendelee na zoezi la uzimaji mitambo ya analojia sehemu zilizobakia. Jopo limeridhika na uandaaaji na usimamizi wa zoezi hili na kwamba kasoro zilizojitokeza ni sababu ya hofu ya mabadiliko na uzoefu wa walaji kwenye matumizi ya visimbuzi. Vilevile kuna faida nyingi za mfumo wa kidijiti ambazo watoa huduma wanatakiwa kuzitumia ili kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Serikali inashauriwa kutoa punguzo la kodi kwa visimbuzi ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi kununua visimbuzi na kupata habari kwa njia ya Luninga

Naomba niwakabidhi ripoti hii ambayo ina maelezo na taarifa za kina kuhusu zoezi tathmini hii.

Imetolewa na:

Prof. Nerey Mvungi        Mtaalamu wa Mawasiliano ya ki electronic
Dr.Francis Sichona         Mtaalamu wa Takwimu
Mr.F.M Ishengoma        Mtaalamu wa Habari na Mawasiliano

JOPO LA WATAALAMU TOKA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
19 FEBRUARI 2014